Msomaji huyo wa Qu’ani wa Iraq aelezea Umuhimu wa Mashindano ya Qur’ani kwa Vijana
Akizungumza na IQNA pembezoni mwa raundi ya mwisho ya mashindano hayo huko Mashhad, Ahmad Razaq Al-Dalfi aliongeza kuwa mashindano kama haya pia yanahimiza kuelewa maana ya maneno ya Mwenyezi Mungu na kuimarisha utamaduni wa vijana wa Qur’ani.
"Mtu yeyote anayejifunza Qur’ani amepata kila kitu na anajenga tabia imara kupitia mafundisho ya Mwenyezi Mungu," alisema, na akiongeza kuwa na elimu ya sayansi za Qur’ani kunamaanisha kuwa hakuna upotofu, vita vya kisaikolojia, au athari zisizo za kimaadili zitakazoweza kumwathiri.
Alibainisha kuwa moja ya faida za kuandaa mashindano haya ni kuendeleza shughuli za Qurani, kuwahamasisha vijana kujifunza Qur’ani, pamoja na kuibua vipaji ambavyo havikupata fursa ya kuonekana hadi sasa.
Aidha, Al-Dalfi alisema kuwa kukusanyika kwa wawakilishi kutoka mataifa tofauti kwa ajili ya Qu’rani hujenga mahusiano na urafiki miongoni mwao, huku kusikiliza Qur’ani kuleta uponyaji wa nyoyo.
Pia alisifu hali maalum ya kiroho katika mashindano haya kutokana na kuandaliwa katika maeneo matukufu ya kaburi la Imam Ridha (AS).
Safari Yake ya Qur’ani Tukufu
Alipoulizwa kuhusu safari yake ya kujifunza Qur’ani, msomaji huyo wa Iraq alisema:
"Tangu utotoni, nilianza kujifunza Qur’ani kutoka kwa wazazi wangu na walimu wangu, na kwa neema ya Mwenyezi Mungu, niliweza kuiweza Qur’ani Tukufu hatua kwa hatua ndani ya kipindi cha miaka 6-7."
Kuhusu mtindo wake wa usomaji, alisema:
"Masheikh mashuhuri ninaowaiga ni Sheikh Mustafa Ismail, Sheikh Abdul Basit Abdul Samad, Sheikh Minshawi, na Sheikh Shahat Muhammad Anwar, ambao ni wasomaji mashuhuri wa Misri. Miongoni mwa wasomaji wa Iraq, ninaiga Sheikh Osama Al-Karbalayi, na miongoni mwa wasomaji wa Iran, ninafuata Master Karim Mansouri."
Wasomaji na wahifadhi wa Qur’ani kutoka mataifa 144 walishiriki katika raundi ya awali ya Mashindano ya 41 ya Kimataifa ya Qur’ani Tukufu ya Iran, ambapo wawakilishi wa mataifa 27 wamefanikiwa kufikia fainali katika makundi ya wanaume na wanawake.
Fainali hizo, ambazo zinaendelea katika mji mtakatifu wa Mashhad, zitafikia tamati Ijumaa katika hafla ya kufunga mashindano, ambapo washindi wa juu watatangazwa na kutunukiwa zawadi.
Mashindano ya Kimataifa ya Qur’ani Tukufu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huandaliwa kila mwaka na Shirika la Awqaf na Mambo ya Hisani la nchi hiyo.
Lengo lake ni kuendeleza utamaduni na maadili ya Qur’ani miongoni mwa Waislamu na pia kuonyesha vipaji vya wasomaji na wahifadhi wa Qur’ani hiyo Tukufu.